Polisi wamefungua uchunguzi dhidi ya mchungaji na wafuasi wa kanisa la Pentekoste katikati mwa Kenya, wanaotuhumiwa kwa unyanyasaji wa kingono kwa wanawake kadhaa wenye umri wa kati ya miaka 17 na 70.
Polisi waligundua tukio hilo walipokuwa wakichunguza kisa cha kanisa kuchomwa moto katika mji wa Kianjai, takriban kilomita 250 kaskazini mwa mji mkuu Nairobi. “Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa kisa hicho… kilikuwa ni matokeo ya hasira ya wakazi dhidi ya tawi la la Makanisa ya Kipentekoste ya Kenya ya Afrika Mashariki katika eneo hilo,” imeandika polisi katika ripoti iambayo shirika la habari la AFP limepata kopi siku ya Jumanne.
Kulingana na waraka huo, Mchungaji Daniel Mururu aliwaamuru wazee wa kanisa na baadhi ya wasaidizi “kuwavua nguo wanawake na wasichana, kunyoa nywele zao za sehemu ya siri, kunyonya matiti yao na kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake na wasichana hao.”
Polisi wanadai kurekodi taarifa za mashahidi 23 wa vitendo kama hivyo dhidi ya msichana wa miaka 17, ambaye sasa ni mjamzito. Kwa jumla, “zaidi ya wanawake saba wenye umri wa miaka 17 hadi 70 walidai kuwa waathiriwa” wa unyanyasaji wa kijinsia, polisi imeongeza. Kwa mujibu wa polisi, mchungaji na wazee “waliwachochea wafuasi” kwa kuwalazimisha au kuwachochea “kujihusisha na vitendo vichafu”, wakiwaambia kuwa walikuwa katika hatari ya kuugua au kuwa tasa ikiwa hawakufanya hivyo.
Nchi ya kidini, yenye Wakristo wengi katika Afrika Mashariki, Kenya ina maelfu ya “makanisa” – 4,000 yanayoojulikana kiserikali – ambayo wakati mwingine huingia kwenye shughuli za uhalifu. Kenya ilitikiswa mwaka jana na ufichuzi wa “mauaji kwenye msitu wa Shakahola”, na kugunduliwa kwa mamia ya miili ya wafuasi wa dhehebu la mwinjilisti katika pwani yake ya mashariki.