Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, ametangaza kuanza kwa msimu wa Krismasi mnamo Oktoba 1, mwaka huu, akidai kuwa ni njia ya kuleta furaha na amani kwa taifa.
Tangazo hili la kushtukiza, ambalo limewahi kutolewa mapema zaidi kuliko miaka iliyopita, linakuja wakati ambapo nchi hiyo inakabiliana na mgogoro mkubwa wa kisiasa na ukandamizaji wa upinzani.
Katika kipindi chake cha kila wiki cha televisheni, Maduro alisema, “Septemba inanukia Krismasi!” Akifurahia kwa sauti, aliwahakikishia wananchi wake kuwa sherehe hizo zitaleta amani, furaha, na usalama kwa wote,hata hivyo, hatua hii inaonekana kuwa mkakati wa kisiasa wa kudhibiti upinzani na kuhamasisha upendo wa taifa wakati ambapo hali ya kisiasa nchini imezidi kuwa mbaya.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona tangazo hili la Krismasi ya mapema kama njia ya Maduro kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuhamasisha uzalendo, wakati ambapo maelfu ya wananchi wa Venezuela wanatarajia kukumbana na msimu wa sikukuu wakiwa gerezani au chini ya udhibiti mkali wa serikali.
Kwa baadhi, huu ni ushahidi mwingine wa jinsi serikali inavyotumia mbinu za kihisia ili kuficha changamoto kubwa zinazoikabili nchi hiyo.