Papa Francis, katika jitihada zake za kujenga madaraja kati ya dini mbalimbali tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, ametembelea msikiti mkubwa zaidi katika taifa lenye Waislamu wengi duniani, Indonesia, kisha kutoa tamko la pamoja na Imam Mkuu wa Indonesia, Nasaruddin Umar, akitaja matatizo mawili makubwa yanayoukabili ulimwengu ambayo ni watu kutokuwa na utu, pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
“Tatizo la ulimwengu la kutokuwa na utu linaonyeshwa hasa na vurugu na migogoro inayosababisha idadi kubwa ya waathirika,” lilisema tamko hilo lililosainiwa katika mji mkuu, Jakarta.
Aidha Papa alisisitiza wasiwasi wake juu ya jinsi dini inavyotumika vibaya kuleta mateso kwa wengi, hasa wanawake, watoto, na wazee, akisema kuwa jukumu la dini linapaswa kuwa kukuza na kulinda heshima ya kila maisha ya binadamu.
Kuhusu mabadiliko ya tabianchi, tamko hilo lilieleza kuwa matumizi mabaya ya rasilimali, yameleta athari hasi kama vile majanga ya asili, ongezeko la joto duniani na mifumo ya hali ya hewa isiyotabirika, ambayo ni kikwazo kwa kuishi kwa amani kati ya watu.
Ziara ya Papa katika Msikiti wa Istiqlal, ambao uko karibu na Kanisa Kuu la Kikatoliki la jiji hilo, inaonyesha nia yake ya kuimarisha mahusiano kati ya dini mbili hizo.
Katika tukio hilo, Papa alisikiliza sala za Kiislamu zikisomwa na msichana kipofu anayeitwa Syakila, mshindi wa shindano la kitaifa la usomaji wa Quran. Ziara yake pia imeangazia jumuiya ya Wakatoliki milioni 8.6 nchini Indonesia na jamii nyingine za wachache, akiwapa matumaini na kuimarisha imani yao.