MKOA wa Geita unatarajiwa kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kitaifa ya Maulid ya kuzaliwa mtume Muhammad usiku wa Septemba 15 kuamukia Septemba 16, viwanja vya CCM kalangalala mjini Geita.
Hayo yameelezwa na Shehe wa Mkoa wa Geita, Alhaji Yusuph Kabadi mbele ya waandishi wa habari na kueleza Maulid hayo yatatanguliwa na wiki ya Maulid ambayo itaanza Septemba 09.
Shehe Kabadi amesema Maulid hiyo inatarajiwa kuwa ya kimkakati na itafahamika kama Maulid ya Dhahabu ambayo itakutanisha makundi ya viongozi wa kidini kutoka nchi nzima.
“Hii ni kwa sababu mkoa wetu wa Geita kama mnavyofahamu ni mkoa wenye madini ya dhahabu, tunataka watu waje wajionee na kushuhudia fadhila za mwenyezi Mungu,” amesema Kabadi.
“Mgeni rasmi katika Maulidi ya kitaifa anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania na mgeni rasmi katika Baraza kuu la Maulid kitaifa anatarajiwa kuwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan,” amesema Kabadi.
Katibu Bakwata Mkoa wa Geita, Abbas Mtunguja amesema Mufiti wa Tanzania, Shehe Abubakar Zubeir bin Ally anatarajiwa kuwasili Geita kupitia uwanja wa ndege Chato siku ya Septemba 12.
Amesema baada ya kuwasili Mufiti atazuru kaburi la Hayati Dk John Magufuli na kasha kwenda kuzindua jengo la msikiti uliojengwa na Naibu Waziri Mkuu Dk Dotto Biteko Ushirombo wilayani Bukombe.