Takriban wanafunzi 17 wamefariki dunia huku wengine 14 wakijeruhiwa kufuatia moto uliozuka kutoka kwenye bweni la shule ya msingi katikati mwa Kenya. Moto huo ulitokea usiku wa kuamkia leo katika shule ya Hillside Endarasha huko Kieni, katika kaunti ya Nyeri, Resila Onyango, msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi ya Kenya alisema. Aliongeza miili yao imechomwa kiasi cha kutoweza kutambulika.
Msemaji wa polisi Resila Onyango amethibitisha tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa wanafunzi wengine 14 wamejeruhiwa vibaya, na wamekimbizwa hospitalini.
Inaelezwa kwamba moto huo ulianza usiku wa kuamkia leo wakati wanafunzi hao wakiwa wamelala kwenye bweni lao.
“Kuna wanafunzi 17 ambao wamethibitishwa kufariki wakati wengine wakiwa wamepelekwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya.” amesema msemaji wa polisi Resila Onyango.
Licha ya kuthibitisha mkasa huo, maofisa wa polisi hawajatoa maelezo kuhusu umri wa waathiriwa wa mkasa huo.
Aidha msemaji huyo wa polisi ameeleza kwamba miili ambayo imeondolewa kwenye eneo la mkasa imechomeka kiasi cha kutotambulika.