Dozi zaidi ya laki 1 za kukabiliana na virusi vya Mpox zimewasili nchini DRC, hii ikiwa ni awamu ya kwanza kwa nchi hiyo kupokea chanjo za ugonjwa huu, dozi nyingine laki 1 zikitarajiwa wikendi hii.
Dozi hizi ni sehemu ya chanjo zaidi ya laki 2 zilizonunuliwa na umoja wa Ulaya, ambao ulisema utazigawa kwa nchi za Afrika ambazo zimeathiriwa zaidi na maambukizo ya Mpox ikiwemo DRC.
Aidha umoja wa Ulaya unatarajia kununua dozi nyingine zaidi ya laki 3 na kuzitoa kwa nchi za Afrika ambapo itafanya ukanda huo kuwa umechangia chanjo zaidi ya laki 5 na elfu 60 za mpox.
Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO, mchakato huu ni sehemu ya mpango wa umoja wa Ulaya unaolenga kuzisaidia nchi wanachama kukabiliana na msambao wa virusi hivyo hatari, ambavyo vimetangazwa kuwa janga la kimataifa.
Zaidi ya euro milioni 9 tayari zimetengwa na umoja wa Ulaya kukisaidia kituo cha udhibiti wa magonjwa barani Afrika CDC, kuratibu kampeni ya upatikanaji wa chanjo kwa haraka kwa nchi wanachama.