Utawala wa Rais Joe Biden umetangaza hatua kadhaa zinazolenga kukabiliana na kile inachosema ni juhudi zinazoungwa mkono na serikali ya Urusi kushawishi uchaguzi ujao wa rais wa Marekani.
Hizi ni pamoja na mashtaka ya jinai dhidi ya raia wawili wa Urusi, kunasa vikoa 32 vya mtandao, na vikwazo dhidi ya watu na mashirika 10.
Maafisa wa Marekani wanasema lengo la Moscow ni kuzidisha mgawanyiko wa kisiasa nchini Marekani na kudhoofisha uungwaji mkono wa umma kwa msaada kwa Ukraine katika vita vyake na Urusi.
Mwanasheria Mkuu Merrick Garland alisema hatua hizo zinahusiana na matumizi ya Urusi ya vyombo vya habari vya serikali kuorodhesha washawishi wa Kimarekani wasiojua kueneza propaganda na habari potofu.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya viongozi wa RT, shirika la vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.
Wasiwasi mwingi unaoizunguka Urusi unajikita kwenye mashambulizi ya mtandaoni na kampeni za kutoa taarifa zisizo sahihi zilizoundwa kushawishi kura ya Novemba.
Mbinu hizo ni pamoja na kutumia vyombo vya habari kama vile RT kuendeleza ujumbe na maudhui dhidi ya Marekani, pamoja na mitandao ya tovuti bandia na akaunti za mitandao ya kijamii zinazokuza madai na kuyaingiza katika mazungumzo ya mtandaoni ya Wamarekani.
Kwa kawaida wanashikilia mada za kisiasa zenye mgawanyiko kama vile uhamiaji, uhalifu, ajira, au vita huko Gaza.
Mara nyingi, raia wa Marekani wanaweza wasijue kuwa maudhui wanayoona mtandaoni yalitoka au yalikuzwa na Kremlin.