Kiongozi wa upinzani wa Uganda Bobi Wine ameungana na wananchi wenzake kuomboleza kifo cha mwanariadha Rebecca Cheptegei aliyefariki Alhamisi asubuhi.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, kiongozi huyo wa chama cha National Unity Forum (NUP) alilaani mazingira ya kifo cha mkimbiaji huyo wa mbio za masafa marefu.
Wine alibainisha kuwa kifo cha Cheptegei kilimhuzunisha sana na sasa anaomba haki ifuatwe ili mhusika/wahusika waadhibiwe.
“Nimehuzunishwa sana na kifo kisichotarajiwa cha mwanariadha huyu mdogo na mwenye kipaji kutoka Uganda, Rebecca Cheptegei. Mazingira ya kifo chake yanasikitisha zaidi. Ripoti za awali zinaonyesha alimwagiwa petroli na mpenzi wake wa zamani na kuchomwa moto,” Bobi Wine aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter.
Aliongeza, “Tunatumai kunaweza kuwa na uchunguzi wa haraka na wa ufanisi wa tukio hilo na wahusika kufikishwa mahakamani. Familia na wapendwa wake wapate faraja katika wakati huu mgumu sana.”
Cheptegei alipoteza maisha siku ya Alhamisi asubuhi alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya Moi Teaching and Referral katika kaunti ya Uasin Gishu.
Wakati huo huo, waziri wa michezo wa Kenya, Kipchumba Murkomen alimuomboleza mkimbiaji huyo wa mbio za marathon, akisema kifo chake ni hasara kwa ukanda wote wa Afrika Mashariki.