Shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) limesema kuwa, mafuriko yanayoendelea Sudan Kusini yameshaathiri zaidi ya watu 710,000 katika kaunti 30 kati ya 78 za nchi hiyo.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa, mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyoanza mwezi Mei yamezidisha hali mbaya ya kibinadamu ambayo tangu zamani ni mbaya hasa katika masuala ya uhaba mkubwa wa chakula, kuzorota uchumi, kuendelea migogoro, miripuko ya magonjwa na athari za vita baina ya majenerali wa kijeshi katika nchi jirani ya Sudan.
Tarehe 29 mwezi uliopita wa Agosti, shirika hilo la Umoja wa Mataifa lilikadiria kuwa katika kilele cha msimu wa mvua yaani kati ya Septemba na Oktoba, mafuriko yanaweza kuathiri hadi watu milioni 3.3 katika maeneo yote ya Sudan Kusini, ikiwa ni pamoja na jamii ambazo ndio kwanza zinapata nafuu kutokana na mafuriko makubwa ya 2019-2022, ambayo yalipelekea watu wasiopungua milioni moja kupoteza makazi yao.
Taarifa ya OCHA imeongeza kuwa, mashauriano ya ngazi ya juu yaliyofanyika Juba siku za Jumatatu na Jumanne yalizingatia jinsi Sudan Kusini ilivyojiandaa kukabiliana na mafuriko kupitia mpango uliopangwa kabla ya kukabiliana na mafuriko. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuchukuliwa hatua makini za kushughulikia maafa yanayozidi kuongezeka.