Taasisi ya World Vegetable Center kwa kushirikiana na Crop Trust, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika pamoja na Tume ya Umoja wa Afrika imezindua mkakati kabambe wa kunusuru vinasaba vya mboga mboga za asili ya Kiafrika ambazo uwepo wake unatishiwa kutoweka.
Mpango huo wa miaka 10 umezinduliwa wakati wa mkutano wa mambo ya chakula barani Afrika uliofanyika Kigali nchini Rwanda tarehe 2-6 Mwezi September 2024.
Mkurugenzi mkuu wa World Vegetable Center kwa ukanda wa Afrika Dkt. Gabriel Rugalema alisema mabadiliko ya tabia ya nchi na ukuaji wa miji ni baadhi ya sababu zinazopelekea kutoweka kwa baadhi ya mboga mboga za kiasili za Kiafrika.
“Athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, ukame, mafuriko, ukuaji wa miji ni baadhi ya sababu zinazohatarisha uwepo wa mboga mboga za kiasili za Kiafrika. Mkakati huu wa miaka 10 unalenga kuwaleta pamoja wadau mbali mbali kwa ajili ya kuokoa mboga mboga za kiasili za Kiafrika,” alieleza.
Katika kipindi cha miaka kumi ijayo, kiasi cha dola za Kimarekani milioni 12 kitahitajika kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo. Mpango utagusa maeneo manne ikiwa ni pamoja na kuokoa, uhifadhi, kuandaa na kusambaza mbegu pamoja na taarifa, ushirikiano, kutengeneza sera wezeshi pamoja na elimu.
Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda ambaye alishiriki mkutano na uzinduzi wa mpango huo alihimiza juu ya suala la kupiga vita utapia mlo huku akisisitiza ulaji wa chakula bora ikiwa ni pamoja na kuongeza mboga mboga katika mlo.
“Uelewa juu ya aina mbali mbali za mboga mboga za kiasili zimepotea kwa jamii nyingi za kiasili za Kiafrika. Afrika ni nyumbani kwa aina nyingi za mboga mboga ambazo uwepo wake unatishiwa kutoweka haswa kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na ukuaji wa miji. Kwa mfano aina ya cowpeas ambayo ni ya mwituni ikiwa na asili ya Afrika tayari imeshatoweka,” alisema Dkt. Sognigbe N’Danikou,ambaye ni mwanasayansi na mtafiti kutoka World Vegetable Center.
Alisema mpango huo pamoja na mambo mengine utakusanya mbegu za aina mbali mbali kiwa ni pamoja na hizi za mwituni lengo likiwa ni kuzihifadhi na kuzizalisha. Zaidi ya silimia 90 ya mbegu zinazotumika barani Afrika zinatoka kwa wakulima ambao huhiziifadhi kila wanapovuna. Kama utaratibiu huu utatekelezwa kikamilifu, utasaidia utaratibu wa kuhifadhi mbegu za asili za kiafrika.
Dkt. Sognigbe alisema kuna haja ya kuwekeza kwenye miundo mbinu katika ngazi ya nchi ili kuwepo na benki ya mbegu ambazo zitasaidia kuendeleza upatikanaji wa mbegu na kuondoa uwezekano wa kutoweka kwa mbegu za asili.