Bei ya Chanjo ya mpox inayozalishwa na Bavarian Nordic huenda ikawa changamoto kubwa katika mazungumzo ya kupata Dozi milioni kwa Bara la Afrika, huku kampuni hiyo ya Kidenmaki ikikabiliwa na shinikizo kubwa la kushusha bei yake.
Dozi zaidi ya 200,000 zimewasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini mazungumzo yanayoongozwa na mashirika kama UNICEF yanaendelea kwa lengo la kupata Chanjo zaidi kwa nchi zilizoathirika. Mikataba ya awali inatarajiwa kukamilika ifikapo katikati ya Septemba.
Bavarian Nordic inatarajiwa kusambaza hadi Dozi milioni 12 ifikapo mwaka 2025, lakini gharama ya Dozi moja ni Dola 100 hadi Dola 141 ambayo gharanma hiyo ni kubwa mno kwa nchi nyingi za Afrika.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa bei hii ni zaidi ya kile Nchi nyingi Barani Afrika zinaweza kumudu, hasa kutokana na changamoto za kiafya kama Kipindupindu, Surua, Malaria, na VVU.
Aidha Helen Rees, Mwenyekiti wa kundi la ushauri la WHO Barani Afrika, amesema kuwa bei hii inafanya Chanjo hiyo kuwa ngumu kupatikana kwa urahisi hata hivyo, Bavarian Nordic inakabiliwa na shinikizo la kushusha bei au kuruhusu Kampuni za kutengeneza Chanjo za bei nafuu kwa wingi.
Wakati majaribio ya Chanjo hiyo kama kinga ya Dozi mbili yamefaulu, kuna mjadala ikiwa Nchi za Afrika zitakubali kutumia Dozi moja ili kupunguza gharama.