Rais Samia Suluhu Hassan amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Askofu Chediel Elinaza Sendoro, wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (ELCT) Dayosisi ya Mwanga, aliyeaga dunia katika ajali ya Gari usiku wa Septemba 9, 2024.
Katika ujumbe aliouweka kwenye akaunti yake ya X (zamani Twitter) @SuluhuSamia, Rais Samia alisema, “Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Askofu Chediel Elinaza Sendoro, Napenda kutoa pole zangu kwa Askofu Mkuu wa ELCT, Askofu Dr. Alex Gehaz Malasusa, maaskofu wote, waumini, familia, jamaa na marafiki.”
Aidha Rais Samia alitoa maneno ya faraja kutoka kwenye Biblia akinukuu Waebrania 13:14: “Kwa maana hapa hatuna mji wa kudumu, bali tunatazamia ule ujao.”
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 7:30 usiku katika kivuko cha Himo-Mwanga, ambapo Gari la Askofu liligongana uso kwa uso na Lori la Scania alipokuwa akijaribu kupita magari mengine.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amesema uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo unaendelea huku Mwili wa Askofu Sendoro ukiwa umepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Mwanga kwa mipango yaendelea.
Askofu Sendoro alikuwa askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016 baada ya kugawanywa kwa Dayosisi ya Pare.