Wakulima watatu nchini Afrika Kusini wanakabiliwa na mashtaka mazito ya kuwaua Wanawake wawili na kulisha miili yao kwa Nguruwe, kesi ambayo imezua hasira miongoni mwa umma, Wanaume hao walifikishwa mahakamani Jumanne katika Mkoa wa kaskazini wa Limpopo.
Wamiliki wa Shamba, Zachariah Johannes Olivier, msimamizi Andrian Rudolph de Wet, na mfanyakazi William Musora wanakabiliwa na mashtaka mawili ya mauaji ya kukusudia, jaribio moja la mauaji, na kumiliki silaha kinyume cha Sheria, Musora, raia wa Zimbabwe, pia anakabiliwa na mashtaka ya kuingia nchini humo kinyume cha Sheria.
Kwa mujibu wa madai, mnamo Agosti mwaka huu, Lori la kampuni ya Maziwa lilitupa bidhaa zinazodhaniwa kuwa zimeharibika kwenye Shamba la Olivier, ndipo Wanawake hao, Locadia Ndlovu na Maria Makgatho, waliingia Shambani humo kuchukua bidhaa hizo, ambapo walipigwa Risasi na kuuawa, Mwanaume aliyekuwa nao alijeruhiwa na kufanikiwa kutambaa hadi barabarani kuomba msaada.
Vyama kadhaa vya Siasa viliandamana nje ya Mahakama ya Mankweng Magistrates, wakitaka wakulima hao kunyimwa dhamana na kupewa adhabu kali.
Aidha Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Afrika Kusini ilitoa wito kwa umma kutokuchukua Sheria mkononi kama njia ya kulipiza kisasi, Kesi hii inatarajiwa kuendelea mwezi ujao kwa mujibu wa taarifa zilizopo.