Mgomo wa Wafanyakazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) Jijini Nairobi umesababisha ucheleweshaji na kughairiwa kwa safari za Ndege kwa Abiria wanaoondoka na kuwasili, Shirika la Kenya Airways lilitangaza mapema leo Jumatano.
Mgomo huu, unaoongozwa na Chama cha Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga Kenya, umechochewa na pendekezo la mkataba wa miaka 30 kati ya Serikali ya Kenya na Kampuni ya Adani kutoka India, Chama hicho kinapinga mkataba huo kwa kuamini kuwa utaathiri ajira za Wafanyakazi wa ndani na kuingiza Wafanyakazi kutoka nje.
Aidha Serikali ya Kenya, kwa upande wake, imeeleza kuwa Uwanja wa JKIA unahitaji kuboreshwa kwani unafanya kazi zaidi ya uwezo wake wa sasa, ingawa umesisitiza kuwa Uwanja huo haupo kwenye mpango wa kuuzwa, Serikali pia imesema hakuna uamuzi wa mwisho juu ya ushirikiano wa umma na binafsi (PPP) katika kuboresha miundombinu ya Uwanja huo.
Ktika Picha na Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha mamia ya Abiria wakiwa wamekusanyika nje ya lango kuu la Uwanja wa Ndege huku Wafanyakazi wakiimba, “Adani lazima aondoke”, Wafanyakazi hao pia walionekana wakipiga kelele na filimbi, wakionyesha hasira zao dhidi ya mkataba huo wa ushirikiano.
Aidha Mahakama Kuu ya Kenya iliamuru kusitishwa kwa muda kwa pendekezo hilo, ili kutoa nafasi kwa uchunguzi wa kisheria dhidi ya mkataba wa Adani Group, ambao unahusisha ujenzi wa njia mpya ya Ndege na kuboresha Terminal ya Abiria.