Jeshi la Wanamaji la Senegal limeripoti kuwa idadi ya vifo kutokana na ajali ya Boti ya Wahamiaji iliyozama Pwani ya Senegal imefikia 26, baada ya Miili mingine 17 kupatikana Jumanne.
Boti hiyo ya mbao ilikuwa imebeba zaidi ya Wahamiaji 100 kutoka Mji wa Mbour, Senegal, na ilizama baada ya kusafiri umbali wa kilomita 4 pekee Jumapili, kulingana na taarifa za Shirika la utangazaji la Taifa, Radio Television Senegalaise (RTS).
“Timu za jeshi la wanamaji zimegundua miili 17, Mabaki hayo yalikabidhiwa kwa Vikosi vya zimamoto, jumla ya Miili 26 imepatikana kufuatia ajali hii, na utafutaji unaendelea,” taarifa ya Wanamaji ilisema.
Fukwe za Senegal hutumiwa mara kwa mara na Wahamiaji wa Kiafrika wanaolenga kufika Visiwa vya Canary vya Uhispania, moja ya njia kuu za Wahamiaji wanaojaribu kufikia Ulaya.