WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema sekta ya uvuvi inaingiza mapato ya sh. trilioni 2.94 kwa mwaka na imekuwa ikikua kwa wastani wa asilimia 1.9 kwa mwaka.
“Wastani wa uzalishaji wa samaki kwa mwaka hapa nchini unafikia tani 472,579, huku tani 429,168 sawa na asilimia 91 zikitokana na uvuvi wa kawaida wa kutumia vyanzo vya asili ndani ya bahari, mito na maziwa na tani 43,411 sawa na asilimia tisa zikitokana na ufugaji wa samaki.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Septemba 11, 2024) wakati akifungua Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) wanaohusika na masuala ya Uvuvi, Bahari, Maziwa na Mito ulioanza leo kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu amesema kila siku watu 230,000 wanajishughulisha na uvuvi mdogo na Watanzania takriban milioni sita wamepata ajira zisizo za moja kwa moja kwenye sekta hiyo. “Uvuvi mdogo mdogo unachangia zaidi ya asilimia 95 ya mavuno yote ya samaki nchini,” amesema.
Akielezea fursa za uwekezaji kwenye ufugaji wa samaki, amesema Tanzania ina uwezo mkubwa wa kuendeleza sekta hiyo kutokana na rasilimali kubwa za maji ilizonazo ikiwa ni pamoja na Bahari ya Hindi, maziwa, mito, mabwawa mengi ya asili na yaliyojengwa na binadamu.
“Tanzania ina Eneo Maalum la Kiuchumi (Exclusive Economic Zone – EEZ) la kilomita za mraba 223,000, ambalo ni takriban asilimia 24 ya ardhi yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivi sasa, uvuvi wa kibiashara katika eneo hilo unafanywa hasa na Mataifa ya Uvuvi wa Maji ya Mbali (Distant Water Fishing Nations) chini ya mikataba ya leseni za uvuvi.”
“Eneo Maalum la Kiuchumi la Tanzania ni fursa kubwa ya uwekezaji kupitia ununuzi wa meli za uvuvi, uwekezaji wa huduma za meli, usambazaji wa vifaa vya uvuvi, usambazaji wa chakula (maji, chakula na matunda), kuongeza thamani na usindikaji, utafiti na ulinzi wa baharini na angani.”
Amezitaja fursa nyingine za uwekezaji kuwa ni pamoja na uvuvi wa kina kirefu kwa ajili ya samaki aina ya tuna; kilimo cha mwani; uzalishaji wa vifaranga na chakula cha samaki. “Aidha, kuna fursa kubwa katika eneo la usindikaji wa samaki na miundombinu ya hifadhi ya bahari,” ameongeza.
Akielezea matarajio ya mkutano huo, Waziri Mkuu amesema mkutano huo utatoa mwongozo wa kimkakati kwenye vikao vya juu vya maamuzi vya Umoja wa Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki ili kuboresha usimamizi wa bahari, uvuvi na ufugaji endelevu wa samaki.