Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itaanza kampeni yake ya chanjo ya mpox Oktoba 2, ikiwa ni wiki moja mapema zaidi kuliko ilivyopangwa hapo awali, mkuu wa timu ya kukabiliana na ugonjwa huo amethibitisha.
DRC ambayo ni kitovu cha mlipuko wa mpox ambao Shirika la Afya duniani lilitangaza kuwa hali ya dharura ya kiafya duniani mwezi uliopita, imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa chanjo jambo ambalo lilitatiza kampeni yake ya kudhibiti maambukizo zaidi.
Taifa hilo lilipanga kuzindua chanjo hiyo Oktoba 8 baada ya kupokea dawa yake ya kwanza ya dozi ya mpox wiki iliyopita, hata hivyo mamlaka za afya zinanuia kuanza kampeni ya utoaji chanjo Oktoba 2, amesema Cris Kacita.
“Kuna taratibu ambazo zimebadilika na zimesaidia kumaliza ucheleweshaji,” alisema Kacita, ambaye aliongeza kuwa kampeni ya chanjo itachukua muda wa siku 10 na italenga watu wazima pekee, wakiwemo wataalamu wa afya, walinzi wa mbuga na wafanyabiashara ya ngono katika mikoa sita ya Kongo.