Mafuriko makubwa katika mji wa kaskazini mashariki mwa Nigeria yameua watu 30 na kulazimisha wengine 400,000 kuhama makazi yao, maafisa walisema Jumatano.
“Idadi ya vifo ni 30, msemaji wa idara ya kitaifa ya kusimamia majanga (NEMA) Ezekiel Manzo aliiambia AFP, siku moja baada ya maji kutoka kwenye bwawa lililojaa kusomba maelfu ya nyumba katika mji mkuu wa jimbo la Borno.
Mfanyakazi mwingine wa idara hiyo, Zubaida Umar alisema “Hali huko Maiduguri inatisha sana.”
Alisema mafuriko yaliteketeza asilimia 40 ya mji wote, na watu walilazimika kuondoka kwenye nyumba zao na wametawanyika kila mahali.
Umar alisema takwimu walizonazo ni kwamba kuna watu 414,000 waliohama makazi yao.
Mafuriko ya sasa yanakuja karibu miaka miwili baada ya mafuriko mabaya zaidi nchini Nigeria katika muongo mmoja kuua zaidi ya watu 600 kote nchini.