BARAZA la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetoa ufafanuzi wa kilichobadilika kwenye Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi, ulioanza jana na unakamilika leo.
Katika toleo letu la jana, tulikuwa na habari kuhusu mtihani huo ikiwa na kichwa kilichosomeka “Darasa la VII kuanza leo siku mbili za mitihani mipya ‘migumu'”.
Hata hivyo, katika taarifa yake jana kwa Nipashe, baraza hilo lilisema mabadiliko hayo hayalengi kufanya mtihani huo kuwa mgumu, bali ni mabadiliko ya muundo.
Ofisa Habari wa NECTA, John Nchimbi, alisema kuwa kilichofanyika ni “maboresho ya Fomati ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi”.
Kwa mujibu wa NECTA, jumla ya watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 1,230,780. Kati yao, wavulana ni 564,176 sawa na asilimia 45.84 na wasichana ni 666.604 sawa na asilimia 54.16.
Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Ally Mohamed, alibainisha kuwa kati ya watahiniwa 1,230,780 waliosajiliwa 1,158,862 sawa na asilimia 94.16 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 71,918 sawa na asilimia 5.84 watafanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wanaitumia katika kujifunza.