Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameziagiza sekta zote zilizoguswa kwenye Ripoti ya Jiolojia na Utafiti wa Madini kuyafanyia kazi maeneo yao kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, Nishati, na Madini ili ripoti hiyo ilete tija kwa taifa.
Alisema, matumizi sahihi ya ripoti hiyo yatachangia uwekezaji utakaozalisha ajira katika sekta husika, na sekta ya ardhi itaweza kuweka mpangilio mzuri wa matumizi ya ardhi, kilimo, ujenzi, na makazi, pia kuiwezesha nchi kujikinga mapema na maafa.
Katika kufanikisha agizo hilo, Dk. Mwinyi amesisitiza kwa Wizara ya Maji, Nishati, na Madini kuzipatia haraka nakala ya ripoti hiyo taasisi zote zilizoguswa ili zianze kuifanyia kazi mapema iwezekanavyo
Alibainisha kuwa kupitia ripoti hiyo, nchi itakuwa na uwezo wa kujikinga na maafa kabla ya kutokea, hatua aliyoieleza itathibitisha dhana ya Jiolojia ya Zanzibar kuwa ni kichocheo cha uchumi wa nchi.
Amesema, uzinduzi wa ripoti hiyo utasaidia kuimarisha dhamira ya Serikali ya kuifanya Zanzibar kuwa kituo cha utalii kwani mapango yaliyogundulika kwenye ripoti hiyo yataweza kutumika kama sehemu za vivutio vya utalii baada ya kuimarishwa.
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi ameeleza kufarijika kwake na ushirikiano wa Wizara mbili za SMZ na SMT kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na wataalamu wa ndani kushirikiana na wenzao wa Wizara ya Madini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Taasisi ya Utafiti wa Miamba na Madini (GST) ya Dodoma kufanikisha utafiti na hatimaye kuandaa ripoti hiyo.