Kamishna Jenerali Wa Mamlaka Ya Kudhibiti Na Kupambana Na Dawa Za Kulevya nchini Aretas Lyimo amesema mamlaka hiyo imeanza kufanya uchunguzi wa dawa mpya za kulevya ikiwemo bangi ya kusindikwa aina ya Skanka inayodaiwa kutengenezwa nje ya nchi.
Lyimo amesema hilo jijini Dodoma wakati akizungumza na wamiliki wa nyumba za unafuu za waraibu wa dawa za kulevya (Sober House) ambapo amesema aina hiyo ya bangi akivuta mama mjamzito anaweza kupata mtoto mwenye udumavu, uzito pungufu na uwezo mdogo wa kufundishika.
“Hili la kuibuka kwa dawa mpya sisi tuna divisheni ya sayansi jinai na inawakemia waliobobea katika masuala ya maabara na kugundua dawa zote mpya za kulevya nchini na sasa hivi tumeanza uchunguzi wa kimaabara kuhusuana na Skanka hii kwasababu ni mojawapo ya dawa mpya awali Tanzania zilikuwa haziji watu walikuwa wamezoea bangi lakini hii bangi ya kusindika imeibuka hivi karibuni na inakemikali kubwa sana inaasilima 40 mpaka 60 ndio maana mtu akivuta anakuwa na ukichaa anavurugwa na akili na wengine wanafanya matendo ya ajabu wanabaka Watoto wadogo na kufanya mauwaji lakini pia inamagonjwa ya moyo” Aretas Lyimo
Katika hatua nyingine amewataka wadau na wamiliki wa nyumba za unafuu wa waraibu wa dawa za kulevya kuongeza idadi ya nyumba katika maeneo yenye upungufu ikiwemo wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga ambako idadi ya waraibu imeongezeka.