Urusi imefyatua risasi ndege ya raia baada ya kuikosea kwa kudhani ni Droni ya kamikaze kutoka Ukraine, hali iliyosababisha rubani wa ndege hiyo kutoa wito wa dharura wa msaada.
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Aktiki la Murmansk Nchini Urusi, ambapo Ndege hiyo ndogo ya raia ilishambuliwa na Walinzi waliodhani ni Droni ya kijeshi.
Kulingana na vyanzo vya Urusi, eneo hilo limekuwa katika tahadhari kubwa kwa siku mbili kutokana na mashambulizi ya Droni za maadui, na hivyo kusababisha vizuizi vya safari za anga.
Baada ya vikwazo hivyo kuondolewa, Ndege mbili ndogo ziliruka kutoka mji wa Apatity, na muda mfupi baadaye moja kati ya Ndege hizo, aina ya ATEC 321 Faeta NG, ilipigwa Risasi na Wanajeshi wa ulinzi wa anga huku Rubani wa Ndege nyingine alishuhudia tukio hilo na kutoa wito wa dharura, akieleza kuwa Ndege iliyokuwa ikishambuliwa ilionekana “kujitokeza kwa njia ya kushangaza”.
Ingawa Ndege zote mbili zilitua salama, Ndege iliyoshambuliwa ilipata uharibifu kwenye bawa na taa ya mbele na inadaiwa Wanajeshi wa ulinzi wa anga wa Urusi walikosea kwa kudhani Ndege hiyo ni Droni ya A-22 Flying Fox kutoka Ukraine, inayofanana na Ndege ndogo.
Aidha tukio hilo bado halijapatiwa maelezo rasmi, na hakuna taarifa zaidi zilizotolewa kutoka kwa Marubani au Mamlaka husika juu ya shambulio hilo.