Kamati ya Kudumu Bunge Maji na Mazingira imetembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa Usafi wa Mazingira katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na kuridhika na kasi ya utekelezaji wake.
Akizungumza mara baada ya kutembelea utekelezaji wa miradi hiyo katika maeneo ya Kigamboni na Kinondoni, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswagwa (Mb) amesema Kamati imeridhika na kazi kubwa inayofanywa na Serikali kupitia DAWASA wa kujenga miradi mikubwa na ya kisasa inayolenga kuboresha Usafi wa Mazingira.
Ameongeza kuwa Kamati pia imeridhishwa na mipango iliyopo ya Mamlaka kuondosha majitaka kutoka majumbani ambapo kiasi cha uchafu kinachozalishwa Dar es Salaam kinachakatwa na kurejeshwa ili kuzalisha maji ghafi mbalimbali ikiwemo gesi, hii ni jitihada kubwa na zenye kuunga mkono harakati za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha Usafi wa Mazingira.
“Tunaipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha afya za Wananchi kwa kuboresha Usafi wa Mazingira”‘ amesema Mhe. Kiswagwa.
“Pia tunaipongeza Wizara ya Maji kwa usimamizi mzuri pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ilani ya Chama tawala inayoitaka kuboresha Usafi wa Mazingira kwa wananchi ili kuepukana na athari za magonjwa ya milipuko,” ameeleza.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) ameishukuru Kamati kwa kufanya ziara ya kukagua uwekezaji kwenye miradi ya majitaka kwa kuwa inachagiza jitihadaa za kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 kiwango cha uwekezaji kifikie asilimia 30 katika Usafi wa Mazingira.