Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 54 Nchini Austria amehukumiwa kifungo baada ya kupatikana na hatia ya kumuambukiza jirani yake virusi vya COVID-19, na kusababisha kifo chake, huku hii ikiwa ni mara ya pili kwa mwanamke huyo kuhukumiwa kwa kosa linalohusiana na janga la COVID-19 ndani ya mwaka mmoja, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani.
Aidha Hakimu alimpa adhabu ya kifungo cha miezi minne kilichosimamishwa na faini ya Euro 800 sawa na Shilinigi Milioni 2 za Tanzania kwa kosa la kuua kwa uzembe mkubwa.
Mwathirika, ambaye pia alikuwa Mgonjwa wa Saratani, alifariki kutokana na homa ya mapafu iliyosababishwa na Virusi vya Corona mwaka 2021, na Ripoti ya vinasaba vya virusi ilionyesha kufanana kwa DNA ya Virusi kati ya Marehemu na Mwanamke huyo, ikithibitisha kwamba “karibu asilimia 100” aliambukizwa kutoka kwa Mshtakiwa.
Hakimu alisema kuwa anamsikitikia Mshtakiwa binafsi na kuamini kwamba hali kama hiyo imetokea mara nyingi, lakini bahati mbaya ni kwamba Mtaalamu alithibitisha karibu kwa uhakika kuwa maambukizi hayo yalitoka kwake, hata hivyo, hukumu hiyo bado si ya mwisho na inaweza kukatiwa rufaa.
Mwanamke huyo alihukumiwa pia mwaka jana kwa kosa la kuhusika na janga la COVID-19, lakini alitolewa hatiani kwa kosa la kuua kwa uzembe katika kesi hiyo ya awali.