Kimbunga Yagi kimeua zaidi ya watu 100 Nchini Myanmar huku mafuriko makubwa yakikumba Nchi kadhaa Barani Ulaya, na kusababisha vifo na uharibifu wa mali.
Zaw Min Tun, Msemaji wa serikali Nchini Myanmmar, alieleza katika taarifa kwamba watu 113 wamethibitishwa kufariki, na wengine 64 hawajulikani walipo kutokana na maafa yaliyoletwa na Kimbunga Yagi.
Ikiripotiwa Mabwawa kuvunjika, nyumba zimeanguka, na maeneo mengi yamefurika kutokana na Yagi, Kimbunga chenye nguvu zaidi Barani Asia mwaka huu, na kikiwa tayari kimesababisha vifo vya watu zaidi ya 280 katika nchi za Vietnam, Laos, Kisiwa cha Hainan Nchini China, na Ufilipino kabla ya kufika Myanmar.
Wakati huo huo, barani Ulaya, Mafuriko yaliyosababishwa na Mvua kubwa kutoka Kimbunga Boris yameleta maafa makubwa katika Nchi za Romania, Austria, Poland, na Czechia.
Nchini Romania, Watu watano wamepoteza maisha huku nyumba 700 zikifurika katika Kijiji cha Slobozia Conachi.
Aidha Mzima moto mmoja amefariki nchini Austria wakati wa uokoaji wa Waathirika wa mafuriko, na Mtu mwingine amezama Nchini Poland, Viongozi wa Nchi hizi wakielezea hali kuwa mbaya, huku Kansela wa Austria Karl Nehammer akieleza kuwa hali ni “ya hatari kubwa.”