BARAZA la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limeshauri serikali kuunda tume huru kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa matukio ya watu kutekwa na kuuawa yanayoripotiwa nchini.
Kukiwa na rai hiyo ya BAKWATA, Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa amesema serikali inafanyia kazi changamoto hiyo ya kiusalama, akidokeza kuwa “kuna baadhi wameanza kuleta chokochoko katika taifa”.
Rai ya kuundwa tume huru ya uchunguzi wa matukio ya utekaji na mauaji nchini ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa BAKWATA, Alhaj Nuhu Mruma, wakati wa maadhimisho ya Baraza la Maulid yaliyofanyika kitaifa mkoani Geita kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana Nyankumbu.
Alisema Baraza hilo linaendelea na litaendelea kupinga matukio ya ukatili na utekaji kwa kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kuthaminiwa utu wake.
“Tume hiyo itakapoundwa ikatende haki kwa kuzingatia sheria. Kwa kuwa huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwakani Uchaguzi Mkuu, ni vyema ukafanyika kwa uhuru na haki,” alisema.
Alhaj Mruma pia alitoa wito kwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kushiriki katika uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura pamoja na kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Kiongozi huyo wa BAKWATA pia alitoa wito kwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi kutenda haki na kufuata taratibu zote za uchaguzi.