Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Zanzibar ina kila sababu ya kuanzisha mfumo wezeshi kwenye biashara zinazochipukia zenye uwezo wa kukua kwa haraka ili kustawisha maisha ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipofungua mkutano wa tatu wa pamoja wa taasisi ya Utafiti na Uchambuzi wa Sera za Kijamii na Uchumi Zanzibar, (ZRCP) leo tarehe 17 Septemba, 2024 kwenye ukumbi wa hoteli ya Madinat Al Bahar Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Dk. Mwinyi ameeleza kuwa Zanzibar ina wajasiriamali vijana wenye vipaji wanaochipukia kwenye ujasiriamali, hivyo ni muhimu kuwakuza kwa ajili ya uchumi jumuishi na endelevu wa Taifa.
Halikadhalika, Dk. Mwinyi amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwawekea mazingira bora na rafiki wajasiriamali na wafanyabiashara ili wavumbue biashara zenye faida na kuviendeleza vipaji vyao kwa maslahi mapana ya Taifa.
Kwa upande mwingine Rais Dk. Mwinyi ametoa wito kwa taasisi za Serikali kuzitekeleza kwa vitendo sera na miongozo mbalimbali itakayoanzishwa na ile iliyopo yenye lengo la kusimamia utekelezaji wa maazimio ya kukuza vipaji vya wataalamu kupitia nyanja zote za ubunifu na teknolojia.