Mkali wa Hip-hop Sean “Diddy” Combs amenyimwa dhamana baada ya kukana hatia katika kesi ya ulanguzi wa ngono.
Jaji wa shirikisho la New York alimweka rumande mwanamuziki huyo baada ya waendesha mashtaka kuhoji kuwa alikuwa “hatari kubwa ya kukimbia”.
Bw Combs, 54, alikamatwa Jumatatu jioni, akishutumiwa kwa kuendesha biashara ya uhalifu kutoka angalau 2008 ambayo ilitegemea dawa za kulevya na unyanyasaji ili kuwalazimisha wanawake “kutimiza tamaa zake za ngono”, kulingana na waendesha mashtaka.
Shtaka la kurasa 14 linamshtaki kwa ulaghai, ulanguzi wa ngono kwa nguvu, na usafiri ili kujihusisha na ukahaba.
Iwapo atapatikana na hatia kwa makosa yote matatu, rapa huyo na mtayarishaji rekodi anakabiliwa na kifungo cha miaka 15 hadi kifungo cha maisha jela.
Alikuwa amevalia fulana nyeusi na suruali ya rangi ya kijivu wakati wa kufikishwa mahakamani Jumanne huko Manhattan.
Alipoulizwa na Hakimu wa Mahakama ya Marekani Robyn Tarnofsky jinsi alivyotaka kujibu, Bw Combs alisimama na kusema: “Sina hatia.”
Wakili wa Bw Combs, Marc Agnifilo, alisema timu ya utetezi tayari ilikuwa imezindua rufaa dhidi ya uamuzi wa dhamana ya hakimu, na kusikilizwa kwa kesi hiyo Jumatano.