Mtengenezaji wa chapa ya walkie-talkies (vifaa vya mawasiliano) ya Kijapani inayohusishwa na milipuko iliyolenga Hezbollah ambayo iliua watu 20 nchini Lebanon na kujeruhi mamia ya wengine amesema kuwa haihusiki na kutengeneza vifaa hivyo vya kulipuka, Reuters inaripoti.
“Hakuna jinsi bomu lingeweza kuunganishwa katika moja ya vifaa vyetu wakati wa utengenezaji,” mkurugenzi wa ICOM aliiambia Reuters nje ya makao makuu ya kampuni huko Osaka, Japan, siku ya Alhamisi. “Mchakato huo ni wa kiotomatiki na wa haraka, kwa hivyo hakuna wakati wa vitu kama hivyo,” aliongeza Yoshiki Enomoto.
Mlipuko wa redio za mkono za mawasiliano zilizotumiwa na Hezbollah siku ya Jumatano katika vitongoji vya Beirut na Bonde la Bekaa, ulifuatia mfululizo wa milipuko ya elektroniki ya pager siku ya Jumanne ambayo iliua takriban watu 12, wakiwemo watoto wawili, na kujeruhi wengine 3,000.
ICOM imesema kuwa ilisitisha utayarishaji wa modeli za redio zilizotambuliwa katika shambulio hilo miaka kumi iliyopita na kwamba nyingi kati ya hizo ambazo bado zinauzwa zilikuwa ghushi.
“Ikitokea kuwa ghushi, basi itabidi tuchunguze jinsi mtu alivyotengeneza bomu linalofanana na bidhaa zetu,” alieleza Enomoto. “Ikiwa ni ya kweli, itabidi tufuatilie usambazaji wake ili kujua jinsi iliishia hapo.”