Rwanda imeanza kampeni ya kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Mpox kwa watu 300 walio hatarini zaidi na wanaoishi kwenye mipaka na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hii imekuwa mara ya kwanza kwa chanjo hiyo kutolewa barani Afrika na Rwanda ilianza kampeni hiyo siku ya Jumanne (Septemba 17), kwa mujibu wa Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti magonjwa barani Afrika (CDC Africa).
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa kitovu cha mripuko wa ugonjwa wa mpox barani Afrika ikiwa na karibu visa 22,000 na vifo 700.
Kampeni ya chanjo nchini Kongo itaanza Oktoba 2.
Wataalamu wa afya barani Afrika wanakadiria kuwa bara hilo litahitaji takribani chanjo milioni 10 ili kuzuia mirpuko wa mpox.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, amezihimiza nchi zaidi kuchangia katika kukabiliana na kusambaa kwa mpox.