Takriban wafungwa wagonjwa 1,700 waliachiliwa Jumatatu kutoka katika gereza kubwa zaidi la Congo, waziri wa sheria alisema, kama sehemu ya juhudi za kupunguza magereza yenye msongamano wa watu nchini humo.
Operesheni hiyo ilifanyika katika Gereza Kuu la Makala katika mji mkuu Kinshasa siku ya Jumatatu mchana.
Wafungwa waliokuwa wagonjwa sana walipata huduma ya matibabu ya haraka, huku wengine wakirudishwa nyumbani kwa mabasi yaliyotolewa na wizara ya sheria na kampuni ya serikali, Waziri wa Sheria Constant Mutamba alisema.
Gereza la Makala, gereza kubwa zaidi nchini Congo lenye uwezo wa kuchukua watu 1,500, linawashikilia zaidi ya wafungwa 12,000, wengi wao wakisubiri kesi zao kusikizwa, Amnesty International ilisema katika ripoti yake ya hivi punde ya nchi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, gereza hilo liliwaachilia wafungwa wengine 600 waliokuwa na kesi ndogo ndogo kwa dhamira hiyo hiyo ya kupunguza msongamano wa wafungwa katika gereza la Makala.
Takriban watu 129 walifariki mapema mwezi huu, katik agereza hilo la Makala, katika jaribio la kutoroka jela, wakiwemo wengine waliopigwa risasi na walinzi na askari na wengine walikufa katika mkanyagano.