Iran ilisema Jumanne inaamini kuwa wafanyikazi waliosalia walionaswa na mlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe mashariki mwa nchi hiyo wamekufa, na kusababisha idadi ya vifo katika moja ya maafa yake mabaya zaidi ya kiviwanda kufikia 49.
Afisa wa dharura wa jimbo, Mohammad Ali Akhoundi, alitoa idadi ya waliofariki katika ripoti iliyobebwa na televisheni ya taifa ya Iran kutoka mgodi wa Tabas.
Takwimu za idadi ya wachimba migodi ndani ya mgodi huo wakati huo zimebadilika tangu kuvuja kwa gesi ya methane Jumamosi kuzusha mlipuko kwenye mgodi wa makaa ya mawe huko Tabas, yapata kilomita 540 (maili 335) kusini mashariki mwa mji mkuu, Tehran.
Takriban watu 70 walikuwa wakifanya kazi wakati wa mlipuko huo.
Miili iliyopatikana kufikia sasa haikuonyesha dalili zozote za majeraha ya mlipuko, ikiashiria kuwa wafanyakazi wengi walikufa kutokana na gesi hiyo kabla ya mlipuko huo.
Kesi kama hizo ni za kawaida katika uchimbaji madini, ingawa hatua za kisasa za usalama zinahitaji uingizaji hewa na hatua zingine kulinda wafanyikazi.
Kampuni haikuweza kupatikana kwa maoni yake.