Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameutaka mradi wa shamba la kahawa la kampuni ya AVIV Tanzania Limited Lililopo katika kijiji cha Lipokela, wilayani Songea mkoani Ruvuma kuwashika mkono wakulima wa pembezoni mwa shamba hilo kwa kuwachimbia visima, usambazaji wa miche bora ya mazao ya kahawa, paprika pamoja na pilipili manga ili kuongeza tija katika kilimo.
Mhe. Rais Dkt. Samia amesema hayo tarehe 24 Septemba,2024 katika ziara yake ya kikazi iliyoambatana na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo na kusema kuwa kwa kuwashika mkono wakulima wadogo katika eneo hilo, kampuni hiyo itakuza ujuzi wa uzalishaji, uhifadhi na uvunaji wa mazao hayo na kuwawezesha wakulima hao kunufaika na soko la moja kwa moja kutoka katika kampuni hiyo.
Aidha, Mhe. Dkt. Samia ameutaka uongozi wa mkoa wa Ruvuma kushirikiana na Kampuni ya AVIV katika kuhakikisha inatekeleza majukumu yake kama ipasavyo katika kuongeza tija ya kilimo na kuchangia pato la taifa.
Shamba la kahawa la Kampuni ya AVIV lina ukubwa wa takribani hekta 2000, huku hekta 1000 zikitumika katika uzalishaji wa zao la kahawa, ambapo pia ajira za kudumu takribani 1400 zimetolewa na ajira 5000 kwa msimu wa kilimo.