Mwenge wa uhuru mwaka 2024 unaendelea kukimbizwa Mkoani Kagera ambapo leo umefika Wilaya ya Missenyi kwa ajili ya kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo Wilayani humo.
Ukiwa Wilayani Missenyi umepitia,kuzindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo mradi wa maji Byeju unaotekelezwa chini ya Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) ukigharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili za kitanzania.
Akisoma taarifa ya mradi huo Meneja wa RUWASA Wilaya ya Missenyi Andrew Kilembe amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 90 na Unatarajia kukamilika mapema mwezi October mwaka huu 2024 ambapo utaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru mwaka 2024 Godfrey Mzava ameipongeza RUWASA kwa hatua nzuri waliyofikia na jinsi wanavyopambana kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani kama ilivyo sera ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia amewataka wananchi kuhakikisha wanaitunza miradi hiyo inayoletwa na serikali mahususi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ili iweze kudumu kwa muda mrefu.