WAZIRI wa Fedha, Dkt Mwigulu Nchemba amezitaka Taasisi za Umma ambazo hazijaanza kutumia Mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya umma wa National – e – Procurement System(Nest) ziwe zimeanza kutumia mfumo huo ili kudhibiti mianya ya fedha za serikali kupotea.
Waziri Nchemba ametoa kauli hiyo leo mapema jijini Dar es Salaam wakati akipokea Ripoti ya Tathmini ya Utendaji Kazi ya Mwaka 2023/24 iliyowasilishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa ununuzi wa Umma [ PPRA ]
Aidha, Dk.Mwigulu ameiagiza PPRA kuendelea kutoa mafunzo kadiri inavyotakiwa, ili kuhakikisha watumiaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma wa Kielektroniki Tanzania (NeST) wanakuwa na uelewa zaidi na kuendelea kuutumia ili kudhibiti upotevu wa fedha za miradi.
Waziri Mwigulu alikumbusha kwamba, kwa kushirikiana na PPRA, serikali inatarajia kuboresha matumizi ya fedha za umma na kuongeza uaminifu katika mfumo wa manunuzi, ili wananchi wanufaike zaidi na rasilimali za nchi
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dk Leonada Mwagike amesema kuwa pamoja na mafanikio mengine, Mamlaka ikifanikiwa kuokoa Jumla ya Sh 14.94bn/- kupitia ukaguzi na Sh 2.7tril/- kupitia ufuatiliaji.
Aidha, amesisitiza ili kuendelea kudhibiti upotevu wa fedha za miradi, Mamlaka itaendelea kuzichukulia hatua za kisheria taasisi zote ambazo hazitumii mfumo wa NeST katika ununuzi.