Wizara ya Afya itazindua kampeni ya kitaifa ya chanjo ya polio kuanzia Oktoba 2 hadi 6, 2024, ili kukabiliana na mlipuko wa hivi majuzi wa virusi vya Polio.
Wataalamu wanasema mlipuko mpya unatokana na virusi aina ya cVDPV2.
“Mwaka huu, wagonjwa watano wamethibitishwa, wakiwemo watoto wanne kutoka kambi ya wakimbizi ya Kakuma katika Kaunti ya Turkana na mmoja amepatikana katika Kaunti Ndogo ya Kamukunji, Nairobi,” Wizara ya Afya imesema katika akaunti yake ya X.
Katibu Mkuu wa Afya ya Umma na Wataalamu Mary Muriuki aliwaambia waandishi wa habari kuwa kampeni hiyo ya chanjo italenga zaidi ya watoto milioni 3.8 walio chini ya umri wa miaka mitano.
Amesema kaunti tisa zilizo hatarini zaidi ni Nairobi, Busia, Bungoma, Turkana, Trans Nzoia, Pokot Magharibi, Kiambu, Machakos na Kajiado.
Alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ya kutokomeza ugonjwa huo wa kupooza itafanyika kwa kujuimusiha maafisa wa jamii 107,000.