Nigeria inatarajia kushuhudia maandamano mapya hii leo Jumanne wakati wananchi watapokusanyika kupinga gharama ya maisha.Maandamano hayo yaliyopewa jina la ‘Bila woga Oktoba 1’ yamepangwa kuendana na maadhimisho ya miaka 64 ya uhuru wa Nigeria ambayo yanaadhimishwa Jumanne, Oktoba 1.
Waandalizi waliviambia vyombo vya habari kuwa maandamano yatafanyika katika mji mkuu Abuja, mji wa bandari wa Lagos na katika miji mikuu ya majimbo katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Maandamano kama hayo yalitikisa Nigeria miezi ya Julai na Agosti, huku waandamanaji wakidai kurejeshwa kwa ruzuku ya mafuta, na kukomesha ufisadi serikalini.
Takriban watu 22 waliuawa katika msako mkali wa vikosi vya usalama, kulingana na wanaharakati.
Katika siku yake ya kwanza ofisini, Rais Bola Tinubu alimaliza ruzuku ya mafuta iliyodumu kwa miongo kadhaa ambayo ilisaidia kupunguza bei. Serikali yake pia ilipunguza thamani ya sarafu mara mbili, na kusababisha bei ya karibu kila kitu kupanda.