Naibu Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde ametembelea Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kujifunza mambo mbalimbali kuhusu baraza hilo na kufahamiana na watumishi ikiwemo menejimenti, kwa ajili ya ushirikiano na uongozi bora.
Katika ziara hiyo, Dk Msonde amefanya kikao kifupi na Menejiment ya NCC, ikiongozwa na Mtendaji Mkuu, Dk Matiko Mturi kwenye ofisi za baraza hilo zilizopo Njedengwa, Dodoma na kisha kutembelea kila ofisi ndani ya NCC, ambapo amesalimiana na kufahamiana na watumishi wa baraza.
Aidha, kwenye kikao hicho, Dk Matiko amemweleza Naibu Katibu Mkuu huyo mambo mbalimbali; ikiwemo uanzishwaji wa Baraza la Taifa la Ujenzi, dhumuni lake, majukumu, mikakati ya taasisi kufikia malengo yake, changamoto pamoja na mbinu zinazoweza kutumika kusaidia taasisi hiyo ifikie panapokusudiwa.
Dk Msonde alilitaja Baraza la Taifa la Ujenzi kuwa ni ‘Think Tank’ ya ya Sekta ya Ujenzi na kusema : “Wizara inawaamini (NCC) kama chombo chake cha ufikiri (Think Tank). Hongera! Licha ya changamoto zote mlizo nazo kuanzia kutokuwepo uwiano kati ya idadi ya watumishi na majukumu 15 mliyonayo, bado mnafanya vizuri…”.
Ameitaka NCC kufikiri zaidi kuhusu njia zinazoweza kutumiwa na Serikali kuwawezesha wakandarasi wazawa kutekeleza miradi mingi zaidi ya wageni kwa manufaa yao na serikali kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa dhana zisizo na ushahidi wala ukweli kwamba wakandarasi wa ndani hawawezi, au wakipewa fedha wanazitumia vibaya au kwamba wageni ndio wanauwezo zaidi hazipaswi kushikiliwa bali kupuuzwa kwa kuwa anaamini wakiwezeshwa inavyohitajika wataweza na manufaa yataonekana.
Wakati akipendekeza kuwezeshwa zaidi kwa makandarasi wazawa kutekeleza miradi nchini, Dk Msonde ameliagiza Baraza kupitia, kuchambua na kuangalia maandiko mbalimbali yanayohusu sekta ya ujenzi kuona kama kuna vipengele vinavozuia au kusimama kama kipingamizi kwa wakandarasi wazawa kupata miradi mikubwa ya ujenzi nchini na kuitekeleza.
Amesema kama vipengele hivyo vipo, NCC iishauri wizara kuhusu hilo ili iangaliwe nini kifanyike kuwaondolea vipingamizi hivyo.
“Tufikiri kwa kina, nataka tuumize vichwa kuona tutawasaidiaje kwa sababu Serikali hii ya awamu ya sita chini ya mama Samia Suluhu Hassan inataka kuwatumia wakandarasi wazawa kwa kutumia rasilimali zake. Kusema tunao wengi kwa idadi kama hawatumiki kwenye miradi yao haisaidii. Serikali inataka wanufaike na vya kwao ili nayo inufaike”.
Ushirikiano na ubunifu ni muhimu
Akimalizia, Dk Msonde amesisitiza kuhusu ushirikiano kati ya taasisi na wakala zilizo chini ya wizara ya Ujenzi akisema ushirikiano una nguvu na unasukuma taasisi kusaidiana kwa lengo la kufanikiwa kwa faida ya wote.