Kampuni ya Airplanes Africa Limited (AAL) yenye makao yake Morogoro, imetangaza kuwa ndege tatu za kwanza zilizotengenezwa Tanzania, zinazojulikana kama Skyleader 600, zimeanza rasmi safari zake ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi wa AAL, Bw David Grolig amesema kuwa ndege moja kati ya hizo tatu imetua kwa mara ya kwanza kwenye uwanja Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ikiwa sehemu ya uzinduzi wa kuanza kufanya kazi.
Bw Grolig alithibitisha kuwa kampuni yao imepata kibali kwa mamlaka husika na msuala ya usafiri wa anga na hiyo imefanyika baada ya kuthibitisha ubora wake.
Alisisitiza kuwa ndege ya Skyleader 600 ni ya kisasa, ina ubora wa hali ya juu na inakidhi viwango vyote vya kimataifa na kuruhusiwa kuanza kufanya kazi.
“Tumetengeneza ndege tatu aina ya Skyleader 600 hapa Tanzania, na sasa ziko tayari kuuzwa. Ndege hizi zinatoa suluhisho bora la usafiri kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla, na tunakaribisha wateja wanaopenda kumiliki,” alisema Bw Grolig.
Alifafanua kuwa uamuzi wa kuanzisha kiwanda cha utengenezaji wa ndege nyepesi Tanzania ulitokana na mazingira mazuri ya uwekezaji nchini na utayari wa wananchi kukubali teknolojia na kujifunza ujuzi mpya.
Alisema kuwa ndege hiyo inabeba abiria wawili, pamoja na rubani na inafaa sana kwa wasafiri wa kibiashara wanaofanya safari za umbali mrefu.
“Tulifanya utafiti wa kina kuhusu mahitaji ya wasafiri wa kibiashara ambao mara kwa mara husafiri kwa umbali mrefu. Kutokana na utafiti huo, tulitengeneza ndege ambayo inawawezesha wafanyabiashara kusafiri kwa ufanisi na kuhudhuria mikutano mbalimbali nje ya maeneo yao kabla ya kurejea mjini,” alisema.
AAL ni kampuni ya kwanza Tanzania kutengeneza ndege za aina hii kwa matumizi ya kibiashara na binafsi na pia ikichangia soko la ajira nchini.Alifafanua kwa kusema kuwa gharama za kununua ndege hizo ni nafuu kama kumiliki gari.
“Mafanikio ya mradi huu yanatokana na jitihada za pamoja na za kujituma za timu yetu ya Kitanzania na Czech,” alisema.
Ndege hiyo ilioneshwa hivi karibuni katika Maonyesho ya Watengenezaji wa Bidhaa ya Tanzania (TIMEXPO 2024) yanayoendelea katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).
TIMEXPO 2024, yaliyoandaliwa na Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), yamevutia zaidi ya kampuni 300 za ndani na kimataifa.