Serikali imetenga Bilioni 10 ili kutekeleza mradi wa umeme vijijini (REA) katika vitongoji 90 vya mkoa wa Njombe vitakavyohusisha vitongoji 15 katika kila jimbo la mkoa huo lenye majimbo sita.
Hayo yameelezwa na katibu Tawala mkoa wa Njombe Judica Omary wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapo ambapo amesema mradi huo umekuwa ukisubiriwa kwa hamu na wananchi hivyo ujio wa mkandarasi unapelekea matumaini ya kupata umeme kwenye vitongoji hivyo.
“Hii ni awamu ya kufikisha umeme kwenye vitongoji niwatake wananchi wa Njombe wawe na muitikio mzuri unapoona nyaya zinaletwa pale kwako au nguzo nawe unaweza kujiongeza ukavuta umeme pale kwako” amesema Omary.
Amesema mradi huo utakapomalizika mapema utasaidia mkoa huo kupewa kipaumbele katika kuongeza vitongoji ambavyo bado havina umeme na kumuagiza mkandarasi wa mradi huo kumaliza mradi haraka ili wananchi wafikiwe na huduma ya umeme na waweze kutumia kwa shughuli zao mbalimbali.
Kaimu meneja wa Tanesco mkoa wa Njombe Veronica Chatanda amesema mkoa wa Njombe una jumla ya vitongoji 1840 lakini vitongoji 1080 ndiyo vimefikiwa na umeme.
Amesema vitongoji ambavyo havijafikiwa na umeme kwa mkoa wote ni 756 ingawa upo mradi mwingine unaendelea wa ujazilizi na tayari mkandarasi amewasha vitongoji 80 na vimebaki 130 kufikia idadi ya 210.
“Tunamshuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutupa vitongoji ili kupata umeme katika mkoa wa Njombe na baada ya utekelezaji wa miradi yote mkoa wa Njombe utabaki na vitongoji 536 ambavyo havina umeme” amesema Mwinuka.
Mhandisi Miradi wa Rea mkoa wa Njombe Dunstan Kalugira amesema mkandarasi wa mradi huo alisaini mkataba na wakala wa umeme vijiji Agosti 20, 2024 na anatakiwa kuanza kazi ndani ya siku 14 tangu asaini mkataba huo.
“Ameshaanza kukagua maeneo ya mradi na atamaliza ndani ya mwezi huu tayari kwa kuanza utekelezaji wa mradi ni muhimu wadau wanaonufaika na huu mradi kupata taarifa ili kusaidia kumsimamia mkandarasi wakati akitekeleza kazi hiyo” amesema Kalugira.
Mkandarasi wa mradi huo kutoka China Railway (CRCERG) Palanivel Kandasamy amesema licha ya kuwa mradi huo ni wa miaka miwili lakini watahakikisha unakamilika kabla ya muda ambao wamekubaliana.
“Bado tunaendelea kukagua maeneo ya mradi na ndani ya mwezi tutakuwa tumemaliza tayari kwa kuanza kutekeleza mradi wa kuweka umeme kwenye vitongoji” amesema Kandasamy.
Mbunge wa Njombe Mjini Deo Mwanyika ameishukuru serikali kwa mradi huo kwani awali jambo hilo limekuwa likiwasumbua wabunge kutokana na ahadi ya selikali ya kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote hapa nchini.
“Ukimpa mtu umeme kama umechokoza nyuki kwahiyo kama maeneo mengine haujafika malalamiko ni makubwa zaidi kila mtu anafikiri umeme ukifika kwenye vijiji ndiyo umefika kwenye vitongoji” amesema Mwanyika.