Israeli imeapa kuiwajibisha nchi ya Iran kutokana na hatua ya Tehran kurusha makombora kuelekea ardhi yake, Iran kwa upande wake ikiapa kutekeleza mashambulio makubwa zaidi iwapo italengwa.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu katika taarifa yake amesema kwamba Iran ilifanya kosa kubwa zaidi usiku wa kuamkia leo na kwamba italipia makosa yake. Aidha ameeleza kwamba nchi yake itajibu dhidi ya yeyote anayeishambulia.
Naye Waziri wa ulinzi wa Israeli Yoav Gallant,ameapa pia kuiwajibisha Iran kwa vitendo vyake. Iran ilianzisha mashambulio yake ya pili ya moja kwa moja kuelekea nchini Israeli siku ya Jumanne.
Katika taarifa yake, Iran imesema ilirusha makombora 200 yakiwemo makombora yenye kasi zaidi, hatua ambayo imetajwa kuzua wasiwasi miongoni mwa raia wa Israeli.
Mataifa kadhaa katika Ukanda wa Mashariki ya kati yametangaza kufunga anga zake kutokana na mashambulio hayo ya Iran.
Katika upande wake, Israeli inasema Iran ilirusha makombora 180 ikiripoti pia kuendelea kutekeleza mashambulio katika ngome za Hezbollah mshirika wa karibu wa Iran haswa katika maeneo ya kusini mwa mji wa Beirut.
Israeli ilionekana kuelekeza vita vya kutoka katika Ukanda wa Gaza kuelekea katika maeneo ya kaskazini kwenye mpaka wake na Lebanon ambapo inakabiliana na wapiganaji wa Hezbollah.