Watu 60 wamepoteza maisha nchini Nigeria, baada ya boti iliyokuwa inawasafirisha hasa wanawake na watoto kuzama kwenye mto Niger, Kaskazini mwa nchi hiyo.
Ripoti za maafisa wa serikali katika eneo hilo wanasema, boti hiyo iliyotengezwa kwa mbao, ilikuwa inawasafirisha zaidi ya 300 abiria waliokuwa wametoka kwenye tamasha la kidini la Mawlid siku ya Jumannne wiki hii.
Mwenyekiti wa serikali za mitaa katika eneo la Mokwa Jibril Abdullahi Muregi,amethibitisha ajali hiyo na kuongeza kuwa, abiria wengine 160 wamefanikiwa kuokolewa wakiwa hai.
Ajali za boti hutokea mara kwa mara nchini Nigeria, kwa sababu ya uvunjifu wa sheria ambapo wamiliki huwasafirisha abiria wengi kupita kiasi, lakini pia usalama na ubora wa vyombo hivyo vya usafiri wa majini, huwa hauzingatiwi.
Mwezi uliopita, boti iliyokuwa inawasafirisha abiria kupita kiasi ikiwa na wakulima zaidi ya 50 ilizama kwenye mto Gummi katika jimbo la Zamfara na kusababisha vifo vya watu 40.
Boti hiyo ilikuwa ikirejea Gbajibo kutoka Mundi baada ya sherehe za kila mwaka za Maulid wakati maafa yalipotokea, Muregi alisema katika taarifa yake siku ya Jumatano.
Shughuli za uokoaji bado zinaendelea, alisema.
Bado haikuwa wazi kwa nini mashua hiyo ilizama.
Msongamano na utunzaji duni ndio unaosababisha ajali nyingi za boti kwenye njia za maji za Nigeria.