Milipuko mikubwa ilitikisa kitongoji cha kusini mwa mji mkuu wa Lebanon usiku kucha, na kuharibu sehemu kubwa ya ardhi na kupeleka moshi mwingi kwenye anga.
Wakaazi wa Beirut walisema mlipuko huo ulikuwa mkubwa sana hivi kwamba ving’ora vya magari vililia na majengo yalitikiswa huku ndege za kivita za Israel zikipiga maeneo yenye watu wengi, ikiwa ni pamoja na eneo la uwanja wa ndege wa kimataifa.
Chanzo kilicho karibu na kundi la Hezbollah nchini Lebanon kililiambia shirika la habari la AFP kwamba Israel ilifanya mashambulizi 11 mfululizo katika shambulio lililotajwa kuwa kali zaidi hadi sasa huko Beirut.
Jeshi la Israel halijatoa taarifa rasmi na Hezbollah haijatoa maoni yoyote.
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa Hashem Safieddine wa Hezbollah – ambaye anawezekana mrithi wa kiongozi Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa katika shambulio la Israel wiki iliyopita – ndiye aliyelengwa na mashambulizi hayo ya anga.
Jeshi la Israel pia lilipiga kivuko cha mpaka cha Lebanon cha Masnaa na Syria katika shambulio tofauti, na kukata barabara inayounganisha nchi hizo mbili iliyokuwa ikitumiwa na mamia kwa maelfu ya watu kukimbia hujuma za Israel katika siku za hivi karibuni.
Zaidi ya watu 300,000 – wengi wao wakiwa Wasyria – walivuka kutoka Lebanon na kuingia Syria katika siku 10 zilizopita ili kuepuka kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel, kulingana na takwimu za serikali ya Lebanon.