CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) kimewakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka ndani na nje ya Tanzania katika kongamano linalolenga kujadili dhana ya elimu ya kujitegemea na umuhimu wake katika maendeleo ya jamii.
Kongamano hilo linalofanyika chuoni hapo kwa kushirikiana na Chuo cha VIA cha Denmark, limefunguliwa rasmi leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Dk Willison Mahera.
Akilifungua, Dk Mahera amesema kongamano hilo linatoa fursa ya kuhamasisha taasisi nyingine za elimu nchini kuzingatia umuhimu wa kufundisha elimu inayolenga kujitegemea.
Amesema, “Kupitia kongamano hili, washiriki na wataalamu watachangia katika kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inawaandaa wanafunzi kuwa na uwezo wa kujitegemea, badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa
Dk Mahera alieleza kuwa kongamano hilo linaendana na mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2023, ambayo inasisitiza utoaji wa elimu bora inayolenga kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuleta mabadiliko katika jamii zao.
“Lengo la elimu ni kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi utakaowawezesha kujitegemea. Ndiyo maana Rais Samia aliagiza kufanyika mapitio ya Sera ya Elimu ya mwaka 2014, na sasa tunayo sera mpya inayolenga kutengeneza wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri,” ameongoza Dk Mahera.
Aidha amesema, serikali imeweka mkazo katika ujenzi wa vyuo vya kati vinavyotoa mafunzo ya fani mbalimbali, ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi utakaowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa
Kongamano hilo la siku mbili linawaleta pamoja watafiti, walimu, na wataalamu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, kujadili mada muhimu zikiwemo utoaji wa elimu jumuishi, sayansi na teknolojia, masuala ya kijinsia, ujuzi wa kujitegemea, na uvumbuzi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa MUCE, Profesa Deusdedit Rwehumbiza, alisema kongamano hili lina manufaa makubwa kwa chuo hicho, hasa katika juhudi zake za kuendelea kuboresha mifumo ya elimu na miundombinu.