Serikali imesaini mikataba mitano itakayowezesha kuanza ujenzi wa madaraja 13 katika sehemu za barabara zilizoathiriwa na Mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya katika Mkoa wa Lindi ambapo jumla ya Shilingi Bilioni 140 zitatumika katika utekelezaji huo.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba hiyo Wilayani Kilwa Mkoani Lindi leo Oktoba 07, 2024, Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua ukubwa wa athari ya miundombinu ya madaraja na makalvati katika Mkoa wa Lindi na kutenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kurudisha upya miundombinu hiyo.
“Dhamira ya Mheshimiwa Rais katika Mkoa wa Lindi ni kujenga upya madaraja yaliyoathiriwa katika maeneo yote ili mvua zitakapoanza kunyesha wananchi watakuwa salama na mawasiliano ya barabara yanakuwa ya uhakika”, amesema Bashungwa.
Amesema ujenzi wa madaraja hayo utatekelezwa katika barabara kuu ya Malendego – Nangurukuru – Lindi – Mingoyo na barabara za Mkoa za Nangurukuru – Liwale, Kiranjeranje – Namichiga, Liwale – Nachingwea na barabara ya Tingi – Chumo – Kipatimu.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali ipo katua za mwisho za kusaini mkataba na Mkandarasi kwa ajili ya kujenga upya barabara ya Mtwara – Lindi – Pwani hadi Dar es Salaam ambapo utekelezaji utaanza awamu ya kwanza kuanzia Mtwara – Mingoyo na baadaye kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya awamu ya pili kuanzia Mingoyo hadi Dar – es Salaam.
Bashungwa amemshukuru Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kwa kutoa msukumo wa kuharakisha upatikanaji wa Wakandarasi watakaotekeleza ujenzi wa madaraja na makalvati na amewapongeza Wananchi kwa subira waliyoonesha kipindi ambacho Serikali ilikuwa inatafuta suluhu ya kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya katika Mkoa wa Lindi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu na kuwasimamia Wakandarasi wote waliopata kazi za ujenzi wa madaraja 13 katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya ili waweze kukamilisha kazi kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Akitoa taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mhandisi Mohamed Besta ameeleza kuwa kazi za ujenzi wa madaraja 13 yatatekelezwa kwa muda wa Miezi 10 kwa kufuata taratibu zote za kitaalam na kusimamiwa na Kitengo cha TECU kutoka kwa Wakala huo.