Naibu rais wa Kenya, anayekabiliwa na pendekezo la kuondolewa madarakani ambapo anatuhumiwa kuunga mkono maandamano ya kuipinga serikali mwezi Juni na kuhusika katika ufisadi na makosa mengine, amejitetea na kuthibitisha kwamba atafika mbele ya bunge siku ya Jumanne.
Rigathi Gachagua, katika hotuba yake iliyopeperushwa kwenye runinga siku ya Jumatatu, alimshutumu mbunge aliyetunga hoja hiyo kwa kusema uwongo, akiiita “ya aibu na ya kuhuzunisha.” Hii ni mara ya kwanza anazungumzia hadharani masuala yaliyoibuliwa na mbunge huyo kwa kina.
Naibu rais anatarajiwa kufika mbele ya bunge Jumanne alasiri ambapo alisema “ataendesha utetezi wangu kwa saa mbili.”
Wafuasi na wapinzani wa Gachagua walikabiliana Ijumaa katika vikao vya umma ambapo fomu za ushiriki wa umma zilijazwa.
Naibu rais alitetea unyakuzi wake wa mali, akisema baadhi ya mali zilizoorodheshwa katika hoja ya kumtimua ni mali ya marehemu kaka yake. Alitetea matumizi ya ukarabati wa makazi yake rasmi akisema yalikuwa katika hali mbaya na inahitaji “heshima.”
Siku ya Jumapili wakati wa mkutano wa maombi katika makazi yake, alimwomba Rais William Ruto, wabunge na Wakenya kumsamehe kwa makosa yoyote wakati wa uongozi wake.
Siku ya Jumatatu, alifafanua kuwa msamaha wake haukuwa wa kukiri hatia na aliondoa uvumi kwamba angejiuzulu.
Wabunge wanatarajiwa kujadili hoja hiyo Jumanne na baadaye kupiga kura kabla ya hoja hiyo kuwasilishwa kwa Seneti.
Jumla ya wabunge 291, zaidi ya 117 inavyotakiwa na katiba, walitia saini hoja ya kumtimua kabla ya kuwasilishwa, lakini baadhi yao kutoka eneo la naibu rais wanasema hawaungi mkono tena baada ya kusikia maoni tofauti kutoka kwa wapiga kura wao.