Zambia ilitia saini Mkataba wa Makubaliano (MOU) na China siku ya Jumatatu kuanzisha kiwanda cha kwanza cha kutengeneza chanjo ya kipindupindu katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Awamu ya kwanza ya mradi huo itagharimu dola milioni 37, huku takriban dozi milioni tatu zikitarajiwa kuzalishwa kupitia ubia kati ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Zambia (IDC) na Jijia International Medical Technology Corporation.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo katika Ikulu ya mji mkuu Lusaka, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema alisema maendeleo hayo ni hatua muhimu katika azma ya nchi hiyo kutokomeza ugonjwa huo ambao umeondoa tija kutokana na kuathiri wananchi.
“Pia tunatuma ishara kwamba Zambia, Afrika na dunia zina uwezo wa kufanya kazi pamoja. Zambia lazima iangaliwe kama kituo, kama eneo la kutengeneza soko kubwa. Na ukiangalia idadi ya watu wa Afrika, ni inakua kwa kasi sana,” Hichilema alinukuliwa akisema kwenye televisheni ya taifa.
Hichilema alisema alitarajia mradi huo kuwa wa kibiashara, na kuongeza hakuna nafasi ya urasimu katika utekelezaji wake, kwani ni kuokoa maisha.
Aliongeza kuwa kabla ya utengenezaji huo, China itachangia takriban dozi milioni tatu za chanjo ya kipindupindu.
Kipindupindu ni cha kudumu katika taifa hilo la kusini mwa Afrika, haswa wakati wa msimu wa mvua, na ingawa kinaweza kutibika, pia hugharimu maisha.