Baraza la Seneti la Kenya linakutana kwa ajili ya kuanza kusikiliza hoja ya kuondolewa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Hoja hiyo inamtuhumu Gachagua kwa ufisadi, ukaidi, kuidhoofisha serikali na kuendesha siasa za migawanyiko ya kikabila, miongoni mwa mashtaka mengi ambayo ameyakanusha vikali.
Spika wa Baraza la Seneti, Amason Jeffah Kingi, amesema vikao vya kusikiliza hoja hiyo vimeanza saa tatu asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki.
Baraza hilo lina siku 10 kukamilisha kesi hiyo na kufanya uamuzi kuhusu hoja hiyo, ambayo itahitaji kuungwa mkono na takribani theluthi mbili ya maseneta ili kuidhinishwa.
Iwapo ataondolewa, Gachagua atakuwa naibu rais wa kwanza kuondolewa madarakani kwa njia hiyo tangu hoja ya kuondolewa madarakani ilipoingizwa katika katiba ya Kenya iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010.