Idadi ya vifo vilivyotokana na mashambulizi ya kikatili ya genge moja lenye silaha nchini Haiti wiki iliyopita imefikia watu 109 huku wengine zaidi ya 40 wakijeruhiwa.
Taarifa iliyotolewa jana na mamlaka nchini humo inasema mauaji hayo yalitokea baada ya nyumba na vyombo kadhaa vya usafiri kuchomwa moto kufuatia genge hilo kurusha risasi kwenye mji wa Port Sonde, ulio umbali wa kilomita 100 kutoka mji mkuu, Port-au-Prince.
Mauaji hayo yametokea wakati kikosi maalum cha kimataifa kinachoongozwa na askari polisi wa Kenya, kikijaribu kurejesha udhibiti wa serikali ya Haiti, ambako magenge yenye silaha yametwaa maeneo makubwa ya mji mkuu na mikoani, na kumlazimisha waziri mkuu kujiuzulu mapema mwaka huu.
Naibu mkuu wa wilaya ya Saint-Marc, Walter Montas, alitangaza idadi mpya ya vifo hivyo kupitia redio moja hapo jana, likiwa ongezeko la vifo takribani 40 kutoka ile iliyotangazwa awali na Umoja wa Mataifa.