Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekua miongoni mwa nchi 15 zilizochaguliwa katika Baraza la Haki za Kibinadamu siku ya Jumatano, licha ya pingamizi za upinzani nchini humo.
Benin, Gambia, Kenya na Ethiopia ni nchi nyingine za Kiafrika zilizochaguliwa kwenye Baraza hilo.
Nchi hizo tano zitahudumu kwa miaka mitatu, kuanzia Januari 1, 2025. Katika mkutano huo, hakukuwa na upinzani wowote dhidi ya uchaguzi wa Kinshasa. Kongo ilizoa kura 172 kati ya 190.
Human Rights Watch, mashirika ya kiraia ya Kongo na vyama vya upinzani vilikuwa vimetaja ukandamizaji wa kisiasa, kuwekwa kizuizini kiholela na mauaji kama sababu za kuinyima Kinshasa kiti katika chombo hicho cha mfano lakini chenye hadhi ya juu.
Waziri wa haki za binadamu wa Kongo alisema nchi hiyo itatumia nafasi hiyo kuboresha hali yake ya haki.
Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lilianzishwa mwaka 2006 na lina jukumu la kulinda na kukuza haki za binadamu duniani kote, na kushughulikia ukiukwaji.